Jopo Linalomchunguza Aliyekuwa Jaji Wa Mahakama Ya Juu Philip Tunoi Lakamilisha Vikao Vyake

Jopo linalomchunguza aliyekuwa jaji wa mahakama ya juu Philip Tunoi limekamilisha vikao vyake. Mwenyekiti wa jopo hilo Sharad Rao, alisema jana kwamba hawana mamlaka ya kisheria ya kuendelea na uchunguzi huo kwani jaji huyo amestaafu. Rao alisema jopo hilo lenye wanachama saba lilikubaliana kwa kauli kuto-endelea na uchunguzi huo kuhusu madai ya Tunoi kuhongwa baada ya jaji huyo kustaafu.
Tunoi alistaafishwa tarehe 15 mwezi huu baada ya mahakama ya juu kudumisha uamuzi wa awali ambao uliwahitaji majaji kustaafu wakiwa na umri wa miaka 70. Rao alisema suala la iwapo jaji huyo alistaafishwa kwa njia ifaayo au la halihusu jopo hilo. Hata hivyo aliongeza kusema kuwa jopo hilo litawasilisha ripoti ya uchunguzi wake kwa rais bila kuzingatia uamuzi ulioafikiwa. Jopo hilo lilibuniwa kumchunguza Tunoi baada ya kulaumiwa kwa kupokea hongo la shilingi milioni 200 kutoka kwa gavana wa Nairobi, Dkt. Evans Kidero ili kumpendelea kwenye rufaa ya kupinga uchaguzi wake kuwa gavana iliyowasilishwa na Ferdinand Waititu ambaye kwa sasa ni mbunge wa Kabete.