Joho azuiliwa kuhudhuria halfa ya uzinduzi wa feri ya Mtongwe

Gavana wa kaunti ya Mombasa, Ali Hassan Joho anasema kulikuwa na njama ya kumzuia kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa feri ya mtongwe inayoongozwa na rais Uhuru Kenyatta. Joho ambaye leo asubuhi alizuiwa kuvuka daraja ya Nyali kuelekea kwenye hafla hiyo alilazimika kurejea afisini mwake baada ya maafisa wa kitengo cha GSU kuzingira nyumba yake katika mtaa wa Nyali. Joho alisema alikuwa na nia ya kuhudhuria hafla hiyo kwa sababu serikali ya kaunti ilichangia ukarabati wa feri ya Mtongwe. Shughuli katika kisiwa cha Mombasa zilikwama baada ya maafisa wa upelelezi kuanzisha msako mkali wa magari na watu waliokuwa wakitumia daraja ya Nyali. Maafisa wa vitengo vya rais, Flying Squad na GSU walisimamisha na kukagua kwa kina magari yote huku kukiwa na madai kuwa walinuia kumzuia Joho kuingia mjini humo. Maafisa hao waliwasimamisha na kuwazuilia Joho na mbunge wa Kisauni, Rashid Bedzimba ambao walikuwa wakijaribu kuingia mjini humo wakitumia pikipiki. Maafisa hao walimsindikiza Joho hadi afisini mwake ambako walikita kambi wakishirikiana na maafisa wa kitengo cha kukabiliana na ghasia. Joho alisema hatua hiyo ya maafisa wa usalama ilikuwa ukiukaji wa haki zake za kimsingi. Joho alisema anaheshimu uamuzi wa rais wa kutomruhusu kuhudhuria hafla hiyo lakini ataandaa mkutano wa hadhara baadaye mwezi huu kuzungumzia masuala aliyotaka kuangazia leo. Afisa wa trafiki katika eneo la pwani Emmanuel Okanda hata hivyo alikanusha madai kuwa maafisa hao walipata maagizo ya kumzuia Joho kuhudhuria hafla hiyo akisema ilikuwa shughuli ya kawaida ya ki-usalama.