Jenerali Kibochi aapishwa kuwa Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi

Jenerali Robert Kariuki Kibochi ameapishwa kuwa mkuu mpya wa vikosi vya ulinzi vya humu nchini katika hafla iliyoshuhudiwa na Rais Uhuru.

Akiongea kwenye sherehe hiyo iliyoandaliwa katika ikulu ya Nairobi Jumatatu tarehe 11 Mei, Rais Uhuru Kenyatta alipongeza vikosi vya ulinzi vya humu nchini kwa kudumisha utaalamu ambao umewezesha asasi hiyo kuwa na mfumo dhabiti wa usimamizi wa kazi za maafisa wa vikosi hivyo.

Akisema kuwa mfumo ulioko wa urithi wa kijeshi unabainisha thamani ya kanuni na taratibu, Rais Kenyatta alitoa wito kwa taasisi nyingine za serikali kuiga mfano huo.

Rais alielezea imani kwamba kwa kujitolea, wakuu wapya wa kijeshi wakiongozwa na jenerali Kibochi watalinda mipaka ya nchi hii, huku ikiendelea kukabiliana na changamoto za kisasa za kiusalama na matukio mengine ya kiasilia.

Jenerali Kibochi amechukua uongozi wa vikosi vya ulinzi vya humu nchini kutoka kwa jenerali Samson Mwathethe aliyestaafu baada ya kuhudumu katika wadhifa wa mkuu wa vikosi hivyo kwa muda wa miaka mitano.

Awali, jenerali Kibochi alihudumu katika wadhifa wa naibu mkuu wa vikosi hivyo.