Jaribio La Kumuondoa Gavana Kidero Mamlakani Latibuka

Jaribio la kumuondoa mamlakani gavana wa Nairobi, Evans Kidero, lilitibuka jana alasiri baada ya vurugu kuzuka katika bunge la kaunti na kusababisha kuahirishwa mapema kikao cha jana. Vurugu zilianza wakati mwasilishi wa hoja ya kumtimua Kidero , Samuel Nyaberi Nyangwara, aliposimama kuwasilisha hoja hiyo akiwa ameketi kwenye kiti cha katibu wa bunge badala ya kiti chake kama ilivyo desturi. Baadhi ya wanachama wa bunge la kaunti walipinga hatua hiyo wakidai hoja hiyo iliwasilishwa bila kufuata utaratibu ufaao. Wanachama wa bunge hilo walimdiriki mwasilishi wa hoja hiyo, ambaye anachukuliwa kuwa muasi katika chama cha ODM ajiuzulu ikiwa haridhiki na chama cha ODM. Hata hivyo Nyangwara amesisitiza kwamba utaratibu ufaao ulifuatwa na atawasilisha hoja hiyo Jumanne wiki ijayo. Kwa upande wake kiongozi wa walio wachache katika bunge hilo, Ngaruiya Chege, akitaja ufisadi, utoaji duni wa huduma na kuongezeka kwa deni la kaunti ya Nairobi katika muda wa miaka minne iliyopita, alisema inagwaje jaribio sawa na hilo la kumtimua Kidero mwaka wa 2014 halikufua dafu, wakati umewadia wa kumtimua gavana huyo.