James Oswago Aishtumu Tume Ya Maadili Na Kukabiliana Na Ufisadi

Aliyekuwa afisa mkuu wa tume ya IEBC James Oswago ameishtumu tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi pamoja na kamati ya uhasibu ya bunge kwa kumtafutia makosa na kumfanya kisingizio kwa changamoto zinazoikabili tume ya IEBC. Katika kujitetea, Oswago aliongeza kusema kuwa ununuzi wa vifaa vya BVR haukuwa na kasoro yoyote ingawa vilikosa kufanya kazi katika siku ya uchaguzi.
Hata hivyo katika kujibu tume ya EACC imeyashtumu madai ya Oswago ikisema kuwa uchunguzi kuhusiana na sakata hiyo ulikuwa wa hali ya juu. Kwenye taarifa mkuu wa mawasiliano katika tume ya EACC, Kairichi Marimba alisema kuwa Oswago alipewa fursa zote kujitetea akiongeza kusema kuwa alihojiwa na kuandikisha taarifa yake ya kwanza tarehe 4 mwezi Machi mwaka uliopita katika jumba la Integrity na taarifa nyingine tarehe 26 mwezi Februari mwaka huu kinyume cha matamshi yake ya awali kwamba tume ya EACC haikumhoji na kumpa fursa ya kujitetea. Oswago ameyasema hayo siku moja baada ya tume hiyo kupendekeza kwamba ashtakiwe pamoja na wengine watatu waliotajwa kwenye sakata ya Chicken gate. Hata hivyo tume hiyo haikupata ushahidi wowote wa kuwapata na hatia makamishna wa IEBC akiwemo mwenyekiti wake Issack Hassan, kuhusiana na sakata hiyo.