Jamaa afungwa jela miaka mitatu kwa kuuza nyama ya paka

Mwanamume aliyeshtakiwa kwa kuwauzia nyama ya paka wafanyabiashara wa samosa amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani na mahakama ya Nakuru. Hakimu mkuu wa Nakuru Benard Mararo alimhukumu  James Kimani kifungo hicho baada ya yeye kukiri kosa hilo alipofikishwa mahakamani hapo jana. Hakimu katika uamuzi wake, alimhukumu mshtakiwa kifungo cha miaka miwili ama alipe faini ya shilling laki mbili kwa kosa la kwanza  na kifungo cha mwaka mmoja ama alipe faini ya shilingi elfu-50 kwa kosa la pili.

Kimani alishtakiwa kwa kuwachinja na kuwauzia nyama ya paka wafanyabiashara wasiokuwa na habari  mjini Nakuru. Kimani alisema ameuza nyama ya zaidi ya paka elfu- moja kwa wenye hoteli na wauzaji wa samosa tangu mwaka 2012. Kulingana na sheria kuhusu udhibiti wa nyama, ni hatari kula nyama ambayo haijakaguliwa na pia nyama za wanyama ambao hawajaidhinishwa kuwa chakula cha binadamu. Paka sio mnyama wa kuliwa na wanadamu kulingana na sheria hiyo kuhusu udhibiti wa nyama