Jaji mkuu aonya kufuatia kupunguzwa kwa bajeti.

Tume ya kuwaajiri wafanyikazi wa idara ya mahakama imeonya kwamba huduma za idara hiyo zitaathiriwa pakubwa katika kipindi cha sasa cha matumizi ya fedha za serikali kutokana na kupunguzwa kwa bajeti yake. Kulingana na jaji mkuu, David Maraga, kupunguzwa kwa fedha zilizotengewa idara ya mahakama hadi shilingi bilioni 14.5 kumeachia idara hiyo shilingi milioni 50 pekee za kutekeleza miradi ya maendeleo. Akiwahutubia wanahabari katika mahakama ya juu, jaji mkuu David Maraga ambaye ni mwenyekiti wa tume ya idara ya mahakama alionya kwamba zaidi ya miradi 70 ya kuboresha na kujenga majengo mapya ya mahakama huenda ikakwama kwa ukosefu wa fedha. Jaji mkuu alisema kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya idara hiyo, miradi 41 inayofadhiliwa na serikali ambayo inakaribia kukamilishwa itakwama huku miradi mingine 29 inayofadhiliwa na banki ya dunia ikikumbwa na hatima sawia na  hiyo.

Kadhalika Maraga alikosoa wizara ya fedha kwa kukosa kuongeza muda wa mradi wa kuimarisha utenda kazi wa idara ya mahakama unaofadhiliwa kwa mkopo wa shilingi bilioni 11.5 kutoka banki ya dunia. Aidha huduma za idara ya mahakama zinazotolewa kwa kutumia magari pia huenda zikaahirishwa kote nchini na kutatiza mpango wa kushugulikia malimbikizi ya kesi zilizoko mahakamani.

Jaji mkuu alisema kwamba hatua ya serikali ya kupunguza bajeti ya idara ya mahakama haifai kwa idara hiyo. Idara ya mahakama ilikuwa imeomba shilingi bilioni 31.2 za kufadhili shughuli zake kwa kipindi cha mwaka 2018/2019.