Jacque Maribe na mchumba wake Joseph Irungu kusalia korokoroni kwa siku sita

Mtangazaji wa Televisheni Jacque Maribe na mchumba wake Joseph Irungu watasalia korokoroni kwa muda wa siku 6 zaidi hadi Oktoba tarehe 15, ambapo watahitajika kuitikia kesi. Jaji Jessie Lessit aliagiza kwamba Maribe azuiliwe kwenye gereza la wanawake  huko Lang’ata, naye Irungu apelekwe katika korokoro ya gereza la Industrial Area. Maribe atafanyiwa uchunguzi wa kiakili katika Hospitali ya Mathare. Aidha, Jaji Jessie Lessit aliagiza kwamba Irungu apewe matibabu kutokana na jeraha lililoko kifuani mwake  ambalo anadai alipata kwa kushambuliwa nnje ya makaazi ya Maribe yaliyoko eneo la Lang’ata, Jijini Nairobi.

Wakili wa Maribe Katwa Kigen, alikuwa ameashiria kwamba alikuwa tayari kuitikia kesi siku ya Jumanne na kwamba hapingi uamuzi wa kumfanyia uchunguzi wa kiakili baadaye. Hii ni kufuatia agizo la mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji  kwamba Maribe na mchumba wake washtakiwe kwa mauaji ya mfanyibiashara wa kike mwenye umri wa miaka 29 Monica Kimani. Katika  taarifa yake iliyotolewa mapema Jumanne, Haji alisema ushahidi aliopokea hadi sasa unatosha kuwafungulia mashtaka wawili hao. Maribe amehusishwa na mauaji hayo ya kinyama kwa kuzingatia uhusiano wake na mshukiwa mkuu.