Jacob Zuma ashinikizwa kung`atuka kutoka uongozi wa ANC

Rais wa Afrika kusini  Jacob Zuma anazidi kushinikizwa na wanachama wandamizi wa chama tawala cha ANC kung’atuka kutoka uongozi wa chama hicho.Kwa mujibu  wa mazungumzo yaliofanywa jana ,baadhi ya wanachama hao wanatarajiwa kufanya kikao cha dharura leo kuhusiana na jambo hilo. Mahala pa Zuma  kwenye chama hicho palichukuliwa na kiongozi mpya Cyril Ramaphosa  mnamo mwezi wa Disemba.Kwa mujibu wa wachanganuzi wa maswala ya kisiasa shinikizo hizo lengo lake ni kuepusha mgawanyiko katika chama hicho kabla ya uchaguzi mkuu  mwaka ujao.Wanachama hao wanataka kumwondoa  rais Zuma wakitumia kifungu cha kumvua mamlaka  kwa kuwasilisha hoja bungeni.Zuma anatarajiwa kuondoka mamlakani mwaka ujao baada ya kufanywa kwa uchaguzi mkuu.Umaarufu wa Chama tawala cha ANC ulianza kushuka kwnye awamu ya pili ya utawala wa rais Zuma kutokana na mdororo wa uchumi  na madai ya ufisadi dhidi ya rais Zuma.Ramaphosa ,ambaye kama kiongozi mpya wa chama cha ANC, yuko katika hali nzuri ya  kushinda uchaguzi mkuu ujao na ametoa mwito wa kudumishwa kwa umoja wa chama.Hata hivyo  watanabahi wa maswala ya kisiasa wanasema huenda Ramaphosa na  washirika wake wakamshinikiza Zuma kung’atuka uongozini ,ikiwa hatafanya hivyo kwa hiari.