Ismael atachuana na Albert 17, katika nusu fainali ya makala ya mwaka huu

Mchezaji nambari moja humu nchini na mshindi mara tatu wa mashindano ya Kenya Open, Ismael Changawa, leo atachuana na Albert Njogu mwenye umri wa miaka 17 katika nusu  fainali ya makala ya mwaka huu katika uwanja wa kilabu cha Nairobi.

Licha ya kuanza  vibaya Changawa alijitahidi  huku akimlemea mpinzani wake kutoka Burundi Issa Chuma seti mbili kwa bila na kufuzu kwa nusu fainali ambapo atacheza na mwenzake Albert Njogu.  Njogu mwenye umri wa miaka 17 aliandikisha ushindi wa seti mbili kwa bila dhidi ya Boris Aguma wa Uganda robo fainalini. Mkenya mwengine Ibrahim Kibet  pia alifuzu kwa nusu fainali kwa kumpiku Frank Menard wa Tanzania seti mbili kwa bila za  6-3 na 6-3. Mchezaji huyo anayeorodheshwa wa pili mashindanoni atachuana na  Abdul Shakur wa Burundi aliyemlemea  Mkenya Petty Andanda seti mbili kwa yao. Katika nusu fainali ya akinadada, anayeongoza mashindanoni  Shufaa Changawa  atamenyana na Narindra Ranaivo wa Madagaska naye  Angela Okutoyi akabiliane na Alicia Owegi. Mshindi katika kitengo cha wanaume atatia kibindoni shilingi elfu tisini, naye bingwa katika kitengo cha akinadada atatuzwa shilingi elfu themanini.