IGAD lahalalisha sera ya biashara kwenye mipaka ya wanachama

Shirika la kiserikali la maendeleo-IGAD limeratibisha sera ya kuhalalisha biashara kwenye mipaka ya nchi wanachama ambazo hazikuwa zikinakiliwa na maafisa wa forodhani. Sera hiyo ya kanda kuhusu biashara zisizo rasmi na ile ya udumishaji usalama mpakani ziliidhinishwa jana na mawaziri wa biashara kutoka mataifa wanachama. Maafisa kutoka Kenya, Djibouti, Ethiopia, Sudan,  Sudan Kusini, Somalia na Ugandan walihudhuria mkutano huo ulioandaliwa huko Mombasa ambako walisema sera hizo zitaimarisha uzinduzi wa eneo huru la kibiashara barani Afrika.

Mnamo tarehe 21 mwezi Machi zaidi ya mataifa 40 ya kiafrika yalitia saini mkataba wa kuimarisha biashara  miongoni mwa mataifa ya kiafrika ambayo ilikuwa imefikia asilimia 16. Maafisa waliohudhuria mkutano huo walisema uzinduzi wa sera hizo utapunguza ushuru wa uagizaji bidhaa miongoni mwa mataifa ya kiafrika ambao kwa sasa ni asilimia 6 hali ambayo imefanya iwe nafuu zaidi kuagiza bidhaa kutoka nje ya bara hili.