IEBC yasisitiza uchaguzi utaandaliwa kama ilivyopangwa tarehe 26 mwezi ujao

Tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC inasisitiza kwamba marudio ya uchaguzi wa urais yataandaliwa kama ilivyopangwa tarehe 26 mwezi ujao licha ya kusambaratika kwa mashauri kati ya tume ya IEBC na waakilishi wa muungano wa NASAA� na wale wa chama cha Jubilee. Mwenyekiti wa tume ya IEBC, Wafula Chebukati, alisema hayo jana baada ya waakilishi wa muungano wa NASA kuondoka kwenye mashauriano yalioandaliwa katika ukumbi wa Bomas of Kenya na kulazimu mkutano huo kuahirishwa. Muungano wa NASA ulikilaumu chama cha Jubilee kwa kuwalazimishia marekebisho kwa sheria za uchaguzi. Kwenye taarifa baada ya kuahirishwa kwa mashauri hayo, Chebukati alisikitikia misimamo migumu iliyochukuliwa na waakilishi wa mirengo hiyo miwili ya kisiasa na akawahimiza vinara wa mirengo hiyo kuchunguza uwezekano wa kujiwasilisha binafsi kwa mikutano ya siku za usoni ili kupunguza kujipiga kifua kwa waakilishi wao. Chebukati alisema tume hiyo iko tayari kufanya mabadiliko mradi tu mabadiliko hayo hayaathiri maandalizi wa marudio ya uchaguzi wa urais.