IEBC Inasajili Watu Elfu 2 Kila Siku Katika Kila Kaunti

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC imesema inawasajili takriban wapiga kura elfu mbili kwa siku katika kila kaunty kwenye shughuli ya mwezi mmoja ya kuwasajili wapiga kura iliyoanza jumatatu wiki hii.Akiwaarifu wanahabari jijini Nairobi kuhusu shughuli hiyo inayoendelea,afisa mkuu wa tume ya IEBC, Ezra Chiloba,alisema tume hiyo inatumai kwamba idadi hiyo itaongezeka.

Chiloba alisema kati ya vifaa 7793 vya kuwasajili wapiga kura kielektroniki vilivyotolewa kwa vituo mbali mbali vya kuwasajili wapiga kura, ni vifaa 68 pekee vilivyoripotiwa kuwa na kasoro huku vingine vyote vikifanya kazi vyema.Pia alisema kwamba tume hiyo imeweka vifaa vya akiba vya BVR katika kila eneo bunge.

Hatahivyo, Chiloba alisema tume hiyo haitaruhusu kutumiwa kwa kadi za kusubiri vitambulisho vipya kutumiwa kuwasajili wapiga kura kwasababu ni kinyume cha sheria kwani kadi hizo hazina nambari za vitambulisho vinavyosubiriwa.Afisa huyo mkuu hatahivyo alisema usajili wa wapiga kura vile vile unaendelea katika vituo vya Huduma centre kote nchini.

Tume hiyo vile vile imewaonya wagombeaji uchaguzi kutotumia nembo ya tume ya IEBC kwenye mabango yao ya kampeini kwasababu tume hiyo haiegemei upande wowote.Tume hiyo inakusudia kuwasajili wapiga kura millioni sita wapya.