IEBC yakutana na wagombeaji urais

Tume ya IEBC leo ilikutana na wagombeaji urais kushauriana kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya kampuni ya KPMG iliyokodiwa kuyakinisha sajili ya wapiga kura na pia swala la uchapishaji karatasi za kura. Tume hiyo iliandaa mkutano huo baada ya muungano wa NASA kuibua dukuduku kuhusu zabuni iliyotolewa kwa kampuni ya Al Ghurair yenye makao yake huko Dubai. Katika mkutano huo, rais Uhuru Kenyatta ambaye amepeleka kampeni za Jubilee katika kaunti ya Kericho aliwakilishwa na katibu mkuu wa chama hicho, Raphael Tuju naye mgombea urais wa NASA, Raila Odinga aliwakilishwa na Norman Magaya, Paul Mwangi, Hamida Kibwana na Otiende Amollo. Wagombeaji urais waliofika binafsi kwenye kikao hicho ni pamoja na Ekuru Aukot wa mrengo wa Thirdway, Abduba Dida wa chama cha Alliance for Real Change na wagombeaji huru, Prof Michael Wainaina na Japheth Kavinga. Cyrus Jirongo wa chama cha United Democratic alimtuma mwakilishi. Wakati huo huo, mgombeaji urais wa mrengo wa Third-Way, Ekuru Aukot ameitaka tume ya IEBC kutangua zabuni ya kuchapisha karatasi za kura na kutoa upya zabuni hiyo kwa kampuni ya uchapishaji isiyo na uhusiano na chama chochote cha kisiasa kinachoshiriki kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi agosti. Katika taarifa, Aukot alisema mrengo wake umetamaushwa na mzozo kuhusu zabuni hiyo, jambo ambalo linahujumu mchakato wa uchaguzi huru.