IEBC yakanusha madai kwamba kamishna wake alizuiwa kwenda Marekani

Tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC imekanusha madai kwamba kamishna wake mmoja kwa jina dakta Roselyne Akombe alizuiwa kwenda Marekani jana usiku. Katika ujumbe wake kupitia mtandao wa Twitter, tume ya IEBC imesema safari ya ndege ya dakta Akombe katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta ilicheleweshwa na maafisa ambao hatimaye walimwomba msamaha. Kulingana na tume ya IEBC, kamishna huyo alikuwa akielekea Marekani kwa mkutano rasmi. Aidha tume hiyo ya uchaguzi imesema dakta Akombe anatarajiwa kurejea hapa nchini siku ya jumapili. Yadaiwa dakta Akombe alikuwa akielekea mjini New York jana usiku alipoagizwa kutoka kwenye ndege kutokana na kile kilichotajwa kuwa maagizo ya maafisa wa usalama. Duru zinaarifu kwamba ilibidi ubalozi wa Marekani uingilie kati ili aachiliwe kutoka kizuizini na kusindikizwa katika uwanja wa ndege wa JKIA.