IEBC kukutana na wanachama wa Jubilee na NASA

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC imesema kuwa leo itakutana na wanachama wa muungano wa NASA na chama cha Jubilee. Akiwahutubia wanahabari mjini Naivasha, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati hata hivyo hakutaja wakati ambapo mkutano huo utafanyika. Tume hiyo imesema kuwa mkutano huo utatumiwa kulainisha maswala machache yaliyoibuliwa na pande hizo mbili huku tume hiyo ikiandaa marudio ya uchaguzi wa urais tarehe 17 mwezi ujao. Muungano wa NASA umekuwa ukishtumu tarehe hiyo ya uchaguzi mpya ukisema haukushauriwa huku chama cha Jubilee kikilalamika kuhusu kundi lililobuniwa na mwenyekiti wa IEBC kusimamia uchaguzi huo mpya wa urais.