Idara ya uhamiaji Ghana yawatenga waliobadili rangi

Idara ya uhamiaji nchini Ghana (GIS) imewapiga marufuku watu waliobadili rangi ya ngozi zao au walio na mistari mwilini kushiriki kwenye zoezi kubwa la usajili. Msemaji mmoja wa idara hiyo amesema kwamba hii ni kwa sababu watu walio na alama kama hizo huenda wakatokwa na damu wakati wa zoezi gumu la kuwapa mafunzo. Baadhi ya raia wa Ghana wameshtuku marufuku hiyo na kuitaja kuwa ya kubagua watu wa jinsia fulani. Wale walio na michoro ya Tattoo mwilini, waliosokota nywele au mikunjo ya miguu pia waliachwa. Idara hiyo ya uhamiaji nchini Ghana ilikuwa imepokea maombi elfu-84, baada ya kutangzwa kwa nafasi 500 pekee. Watahiniwa wanafaa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu na pia kuchunguzwa kwa miili yao kikamilifu kama sehemu ya masharti ya usajili. Ni marufuku dhidi ya alama zozote mwilini ambayo imezua ghadhabu kuliko jambo jingine lolote kupitia kwa mitandao ya kijamii. Raia wa Ghana pia walijibu kwa hasira wakati taasisi hiyo ilipofichua kwamba inakusudia kusajili watu 500 pekee, baada ya raia elfu-84 waliopeleka kulipa ada ya dolla 11 kila mmoja ili kupata fomu. Mbunge mmoja nchini humo, Richard Quashigah, amehimiza wale ambao maombi yao yalikataliwa kuishtaki taasisi ya (GIS) kuhusiana na ada hiyo ya maombi.