ICC Kutoa Uamuzi Juu Ya Kesi Dhidi Ya Naibu Rais Ruto Na Mwanahabari Sang

Kitengo cha rufani cha mahakama ya kimataifa kuhusu kesi za uhalifu wa kivita-ICC leo jioni kitatoa uamuzi kuhusu matumizi wa ushahidi uliokanwa kwenye kesi dhidi ya naibu rais, William Ruto na mwana-habari Joshua arap Sang kwenye mahakama hiyo mjini Hague. Kitengo cha mashtaka kwenye mahakama hiyo kilimruhusu kiongozi wa mashtaka, Fatou Bensouda kutumia ushahidi uliokanwa katika kesi ya uhalifu wa kivita dhidi ya Ruto na Sang. Bensouda aliieleza mahakama hiyo kuwa ushahidi wa mashahidi watano ambao tayari wamekana taarifa walizoandakisha ulivurugwa. Lakini mawakili wa Ruto na Sang wamepinga matumizi ya ushahidi huo wakisema kifungu cha 68 cha mkataba wa Roma kinachoruhusu matumizi ya ushahidi uliokanwa hakiwezi kutumiwa katika kesi hiyo. Walisema kifungu hicho kilifanyiwa marekebisho mwaka 2013 wakati kesi hiyo ilikuwa ikiendelea. Katika ombi lake, Bensouda amewataka majaji wa mahakama hiyo kuzingatia kifungu cha 68 au 69 cha mkataba wa Roma. Kifungu cha 69, sehemu ya pili kipengele cha (a), kinaruhusu matumizi ya ushahidi wa awali ulionakiliwa, mradi tu aliyetoa ushahidi huo asiwe mahakamani na kwamba upande wa mashtaka na ule wa utetezi zilikuwa na fursa ya kuchunguza ushahidi huo wakati uliponakiliwa.