I.E.B.C Yaonya Wanasiasa Dhidi Ya Mijadala Potofu Kuhusu Sheria Za Uchaguzi

Tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC imesema mzozo ulioko miongoni mwa wanasiasa kuhusu marekebisho ya sheria za uchaguzi yataathiri uadilifu wa uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka 2017. Tume ya IEBC sasa inatoa wito kwa chama cha Jubilee na mrengo wa CORD kumakinika katika mijadala yao na kutii sheria. Katika taarifa iliyotolewa jana, tume hiyo ya uchaguzi inawalaumu viongozi wa kisiasa kwa kunukuu visivyo baadhi ya vipengele vya sheria hizo za uchaguzi. Tume ya IEBC imesema tofauti iliyopo baina ya wadau wa kisiasa kuhusu maswala muhimu katika shughuli ya uchaguzi haifai, na inaonyesha ukosefu wa nia ya kisiasa ya kushughulikia maswala ya uchaguzi. Hapo jana, mkurugenzi wa halmashauri ya mawasiliano hapa nchini, Francis Wangusi na afisa mkuu wa IEBC, Ezra Chiloba walifika mbele ya kamati ya bunge la taifa kuhusu haki na maswala ya sheria kuelezea haja ya kurekebisha sheria za uchaguzi ili kujumuisha mfumo wa wakaida wa upigaji kura. Wakati wa mkutano huo, ilibainika kwamba kata 2,400 hapa nchini hazijaunganishwa kwenye mtandao ili kufanikisha mfumo wa kielektroniki kama inavyohitajika kisheria, huku kata 1,366 pekee zikiwa na uwezo wa kutumia mfumo huo wa kielektroniki. Tume ya IEBC pia imefutilia mbali madai kwamba wakfu wa mifumo ya uchaguzi unanuia kuingilia uchaguzi mkuu ujao.