Hospitali Ya Moi Referral Yafutilia Mbali Deni La Wagonjwa Kwa Kiwango Kikubwa

Hospitali ya mafunzo na matibabu maalum ya Moi mjini Eldoret imefutilia mbali asilimia-50 ya deni la shilingi milioni-180 linalodaiwa wagonjwa waliotibitiwa hospitalini humo. Afisa mkuu mtendaji wa hospitali hiyo, Dr Wilson Arwasa amewahimiza wale wanaodaiwa bili za matibabu kulipa nusu ya bili hizo kisha hospitali hiyo itawarejeshea vitambulisho vyao vya kitaifa, hati za kumiliki magari na ardhi zinazohifadhiwa na hospitali hiyo. Alisema hospitali hiyo kwa sasa inazuilia vitambulisho elf-34 vya kitaifa. Dr Arwasa alisema hayo jana katika uwanja wa michezo wa Iten alikokabidhi vifaa vya matibabu vitakavyotumiwa na kina mama wajawazito. Akihutubu kwenye hafla hiyo, seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen alisema vifaa hivyo vitasaidia kufanikisha kampeni ya mradi wa Beyond Zero unaodhaminiwa na mama taifa, Margaret Kenyatta. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa seneta wa Nandi, Stephen Sang na mbunge wa Keiyo Kusini, Jackson Kiptanui.