Hatua Ya Naibu Wa Gavana Wa Machakos Huenda Ikaibua Mzozo Baina Yake Na Gavana Dr. Mutua

Naibu gavana wa Machakos Bernard Kiala amewasimamisha kazi mawaziri wawili wa serikali ya kaunti hiyo na afisa mmoja wa ngazi za juu kwenye hatua ambayo itaibua upya mzozo wa uongozi baina yake na gavana wa kaunti hiyo, Dr. Alfred Mutua.

Kiala alisema mafisa hao walisimamishwa kazi kutokana na utovu wa maadili.Wakati huo huo Kiala aliwarejesha kazini maafisa wawili ambao walikuwa wamesimamishwa kazi na gavana Mutua.

Hata hivyo wadadisi wanahoji endapo Kiala ana mamlaka ya kutekeleza jukumu hilo, huku Kiala akitetea uamuzi wake kwa kusema kwamba hajui mahali alipo Dr Mutua kwa muda wa miezi mitatu iliyopita na kwamba Mutua ameshindwa kukabiliana na ufisadi kwenye serikali hiyo.

Mnamo mwezi Oktoba mwaka jana,Dr. Mutua aliwasimamisha kazi mawaziri wa serikali hiyo Larry Wambua na Francis Maliti kwa muda wa miezi mitatu bila kutaja sababu za kufanya hivyo.

Duru za hivi punde zinaashiria kwamba Mutua tayari ameagiza maafisa waliosimamishwa kazi na Kiala warejee kazini.