Hatimaye CORD Na Jubilee Wataja Wabunge Na Maseneta Watakao Shiriki Mazungumzo Dhidi Ya IEBC

Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria ni miongoni mwa wabunge saba walioteuliwa na muungano wa Jubilee kushiriki kwenye kamati ya pamoja ya bunge inayowajumuisha wabunge wa upinzani ambayo itashauriana kuhusu mbinu za kurekebisha tume huru ya uchaguzi na mipaka, IEBC.

Kundi la Jubilee linaloongozwa na seneta wa Meru Kiraitu Murungi sasa litashirikiana na lile la muungano wa CORD linaloongozwa na seneta wa Siaya James Orengo kuanzisha mashauriano kuhusu marekebisho ya kiuchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Wanachama wengine wa Jubilee ni pamoja na seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, seneta maalum Beatrice Elachi, mbunge wa Taveta Naomi Shaban, mbunge wa Kitutu Chache Jimmy Angwenyi na pia mbunge wa Mandera magharibi Mohamud Mohamed. Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Aden Duale amesema kamati itachunguza madai yaliotolewa dhidi ya makamishna wa tume hiyo na itapokea maoni kutoka kwa wadau wote. Ripoti ya kamati hiyo ni sharti iidhinishwe na angalau wanchama tisa na kuwasilishwa bungeni katika muda wa siku 30. Hoja ya kubuni kamati teule ya pamoja kuhusu IEBC sasa itawasilishwa bungeni wiki ijayo.