Hatibu Wa Serikali Erick Kiraithe Atoa Wito Aliyechomewa Gari Mathare Afidiwe

Hatibu wa serikali Erick Kiraithe ameagiza chama kimoja cha kisiasa ambacho wafuasi wake wanashutumiwa kwa kuchoma gari la kibinafsi katika mtaa wa Mathare jijini Nairobi Jumapili iliyopita kumfidia mwenye gari hilo. Akizungumza na wanahabari afisini mwake, Kiraithe alisema serikali haitaruhusu makundi ya wahalifu kuharibu mali ya umma na akatahadharisha kuwa wale watakaokiuka sheria wataadhibiwa. Kiraithe alisema serikali imejitolea kulinda maisha na mali ya Wakenya na kumchukulia hatua kiongozi yeyote ambaye wafuasi wake watajiingiza katika vitendo vya uhalifu. Inakikisiwa kuwa watu wasiojulikana ambao walikuwa wamehudhuria mkutano wa hadhara katika uwanja wa Masinde Muliro, mtaani Huruma walimshambulia mwenye gari hilo wakidai alimgonga kwa gari mmoja wao. Jumapili iliyopita, vyama viwili vya kisiasa viliandaa mikutano tofauti ya hadhara katika eneo hilo. Chama cha ODM kiliandaa mkutano wake katika uwanja wa Masinde Muliro ilhali kile cha Jubilee kilifanya mkutano katika uwanja wa Mlango Kubwa.