Hassan Omar Hassan akata rufaa mahakamani kupinga ushindi wa Ali Hassan Joho

Aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha Wiper, Hassan Omar Hassan amekata rufaa mahakamani kupinga ushindi wa gavana wa kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho kwenye uchaguzi wa mwezi uliopita. Akiongea na wanahabari mjini Mombasa, Omar alisema kaunti hiyo ni mojawapo ya zile zilizokumbwa na dosari nyingi katika uchaguzi huo. Omar ambaye aliwania ugavana wa kaunti ya Mombasa kwa tikiti ya chama cha Wiper alisema Joho ni kiongozi katika muungano wa NASA ambao ulitahadharisha kuhusu dosari hizo. Aidha alitoa wito wa kushtakiwa kwa maafisa wote waliohusika katika dosari hizo. Omar aliyejiuzulu kama katibu mkuu wa chama cha Wiper juma lililopita alitaja uongozi wa chama hicho kuwa hafifu. Kwenye barua yake, Omar alisema hatafanyia muungano huo kampeni wakati wa marudio ya uchaguzi wa urais tarehe-17 mwezi ujao.