Harun Mwau awasilisha kesi kupinga marudio ya uchaguzi

Aliyekuwa mbunge wa Kilome Harun Mwau ameweasilisha kesi mahakamani akitaka tume ya uchaguzi kuzuiwa kuandaa marudio ya uchaguzi wa urais tarehe 26 mwezi huu. Mwau aliwasilisha rufani inayohimiza mahakama kuu kutangua arifa kwenye gazeti rasmi la serikali tarehe 5 mwezi septemba kuhusu marudio ya uchaguzi wa urais. Mbunge huyo wa zamani anasema kwamba tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC na mwenyekiti wake Wafula Chebukati, ambao wameorodheshwa kama washtakiwa kwenye kesi hiyo wananuia kukiuka kanuni za katiba na sheria za uchaguzi kwenye uchaguzi ujao na hatua hii huenda ikasababisha kutanguliwa tena kwa uchaguzi. Anadai kwamba kwa vile mahakama ya juu iliagiza marudio ya uchaguzi, tume ya IEBC itakuwa inakiuka sheria kwa kutoruhusu uteuzi wa wagombea viti kufanywa. Wiki iliyopita tume ya uchaguzi iliratibisha majina ya wagombea uchaguzi wote wa urais walioshiriki kwenye uchaguzi wa mwezi Agosti, isipokuwa Cyrus Jiringo, ambaye ametangazwa kuwa fukara.