Harambee Stars kuchuana na Angola mwezi Juni

Timu ya taifa ya soka Harambee Stars itachuana na Angola katika mechi ya nne ya kirafiki ya kimataifa mwaka huu tarehe nne mwezi Juni mjini Machakos. Stars itatumia mechi hii kujinoa kwa mashindano ya kuwania kombe la taifa bingwa Barani Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani yatakayoandaliwa humu nchini mwaka ujao. Kocha Stanley Okumbi, atanuia kuendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mechi 11 baada ya timu hiyo kutoka sare tasa na Malawi kwenye mechi ya mwisho ya kirafiki ya kimataifa uwanjani Machakos. Kenya itachuana na Sierra Leone katika mechi ya ufunguzi ya kufuzu kwa kombe la mashindano ya taifa bingwa Barani Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani tarehe 10 mwezi Juni, mwaka huu. Aidha, Okumbi anatarajiwa kukitaja kikosi kitakachoshiriki katika mechi hiyo na mipangilio ya siku za usoni. Stars iliandikisha ushindi wake wa kwanza mwaka huu kwa kuishinda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mabao 2-1 mjini Machakos. Awali,timu hiyo ilitoka sare na Uganda Cranes, bao moja kwa moja. Kenya itashiriki kwa mara ya kwanza katika makala ya tano ya mashindano hayo. Timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndio mabingwa watetezi baada ya kuishinda Mali mabao matatu kwa bila, katika fainali iliyoandaliwa jijini Chigali, Rwanda mwaka jana. Mashindano hayo yataandaliwa katika miji ya Nairobi, Meru, Machakos na Eldoret mwezi Julai, mwaka ujao.

A�