Harambee Starlets Wafuzu Kushiriki Fainali Ya Kombe La Akina Dada Barani Afrika

Kenya itakuwa miongoni mwa timu nane zitakazoshiriki katika fainali ya kuwania kombe la akina dada barani Afrika mwaka huu nchini Kameruni baada ya timu ya taifa ya akina dada Harambee starlets kufuzu kwa fainali hizo kwa mara ya kwanza katika historia ya soka humu nchini. Licha ya kutoka sare kwa kufungana bao 1-1 leo katika uwanja wa kimataifa wa Moi Kasarani Warembo hao wa humu nchini walifuzu kwa fainali hizo zinazoandaliwa kila baada ya miaka miwili kwa kuishinda Aljeria kwa ubora wa mabao ya ugenini baada ya kufunga mabao mawili kwenye mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa huko Algiers. Algeria ilienda kifuambele katika dakika ya 23 kupitia kwa bao lililofungwa na Bouheni Naima baadaya kutunukiwa mkwaju wa ikabu katika eneo la langoni. Hata hivyo, Cherish Avilla Salano aliibuka mchezaji bora mchuanoni baada ya kuisawazishia Kenya na kuifanya idadi ya mabao kuwa moja kwa moja. Fainali za kombe la bara Afrika kwa akina dada zitaandaliwa jijini Yaounde, Cameroon kuanzia tarehe 19 mwezi Novemba hadi tarehe tatu mwezi Disemba mwaka huu.