Harambee Starlets kuchuana na Ghana Jumamosi hii

Timu ya taifa ya soka ya wasichana wasiozidi umri wa miaka ishirini imeratibiwa kuchuana na timu ya Ghana Jumamosi hii, katika mechi ya marudiano ya kuwania tikiti ya kushiriki katika fainali za kombe la dunia.

Mechi hiyo itachezwa katika uwanja wa Kaunti ya Machakos. Timu ya Kenya itanuia kuandikisha ushindi kufuatia ushinde wa mabao matano kwa bila dhidi ya Ghana katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa mwanzoni mwa mwezi huu, uwanjani Cape Coast. Kenya ilikuwa imeishinda Botswana mabao saba kwa moja kisha ikaipiku Uhabeshi mabao manne kwa matatu lakini ikasalimu amri dhidi ya Ghana. Timu ya Kenya inawajumwisha mlindalango Lilian Awuor, walinzi Foscah Nashivanda, Leah Cherotich, Lucy Akoth, Wincate Kaari, viungo Corazon Aquino, Diana Wacera, Stella Anyango, Jentrix Shikangwa, Quinter Atieno na Martha Amunyolete. Fainali za kombe la dunia kwa wasichana wasiozidi umri wa miaka ishirini, litaandaliwa nchini Ufaransa kuanzia tarehe 5 hadi 24 mwezi Agosti, mwaka ujao.