NTSA ,shule za udereva zalaumiwa kwa ongenzeko la ajali

Chama cha wenye matatu kinawalaumu wasimamizi wa shule za kutoa mafunzo ya uendeshaji magari pamoja na halmashauri ya uchukuzi na usalama kwa ongezeko la ajali za barabarani. Haya yamewadia huku serikali ikifutilia mbali leseni za muda zilizoruhusu magari ya uchukuzi wa umma yanayophudumu mijini kuwapeleka abiria kwenye sehemu za mashambani. Mwenyekiti wa chama cha wenye matatu Dickson Mbugua anawashutumu wasimamizi wa shule za udereva kwa kupendekeza kutolewa vyeti kwa madereva ambao hawajakamilisha mafunzo yao. Alisema halmashauri ya uchukuzi na usalama imetoa mtaala wa mafunzo kwa shule zote za uendeshaji magari ambao unapasa kukamilishwa kwa muda wa miezi miatatu lakini maagizo hayo hayajakuwa yakizingatiwa. Mbugua alishutumu baadhi ya maafisa wa halmashauri hiyo kwa utepetevu baada ya maafisa hao kuhusishwa na ajali mbili zilizotokea mwezi huu. Kwenye tukio la hivi majuzi, watu watatu walifariki wakati wa ajali iliyotukia katika eneo la Yatta kwenye barabara ya Nairobi-Garissa huku walioshuhudia wakidai maafisa wa halmashauri hiyo walikuwa wameruhusu basi hilo kuendelea na safari licha ya kulinasa likiwa limebeba abiria wengi kupita kiasi.