Hakainde Hichilema aachiliwa huru

Kiongozi wa upinzani nchini Zambia Hakainde Hichilema, aliyekabiliwa na mashtaka ya uhaini ameachiliwa huru. Chama chake kilisema Hichilema na washtakiwa wenzake 5 waliachiliwa kutoka gerezani na mashtaka ya uahini kutupiliwa mbali. Hichilema alikamatwa mwezi Aprili baada ya msafara wake wa magari kudaiwa kuzuia msafara wa magari wa Rais Edgar Lungu wakati viongozi hao wawili walipokuwa wakielekea kwenye sherehe moja ya kitamaduni magharibi mwa Zambia. Alishtakiwa kwa kuhatarisha maisha ya Rais huyo. Katibu mkuu wa jumuiya ya madola Patricia Scotland alikuwa nchini Zambia wiki iliyopita na akakutana na Rais Lungu na Hichilema. Baadaye alieleza kwamba huenda Hichilema akaachiliwa huru kwa kuzingatia maslahi ya umma.