Geoffrey Kirui na Edna Kiplagat kutetea taji zao za mbio za marathoni,Baston

Wanariadha wa Kenya, Geoffrey Kirui na Edna Kiplagat, wamethibitisha kuwa watatetea taji zao za mbio za marathoni za jijini Boston tarehe 16 mwezi Aprili, mwaka ujao.
Kirui alishiriki katika mbio hizo kwa mara ya kwanza mapema mwaka huu na kupambana dhidi ya wanariadha wengi mahiro. Aidha, alionesha ushupavu wake katika mbio hizo zilizokuwa zake za tatu za masafa marefu, huku akiwa Mkenya wa kwanza kunyakua taji ya mbio hizo tangu mwaka 2012. Miezi minne baadaye, kwenye mashindano ya dunia jijini London, Kirui alitwaa nishani ya dhahabu ya mbio za marathoni. Mwenzake Edna, aliyeshiriki kwenye mbio za jijini Boston kwa mara ya kwanza mwaka huu, alitichomoka kukiwa kumesalia kilomita kumi na kuwazidi kasi wakinzani wake huku akishinda kwa muda wa saa mbili, dakika 21 na sekunde 52, muda wa nne bora katika historia ya mbio hizo. Baada ya mbio hizo za Boston, bingwa huyo mara mbili wa dunia alishiriki mashindano ya dunia kwa mara ya nne na kunyakua nishani ya fedha. Edna, alikamilisha msimu wake kwa kumaliza wa nne kwenye mbio za marathoni za jijini New York, mwezi jana.