Gavana wa Nairobi Mike Sonko aahidi kutoa mifuko isiyoathiri mazingira

Gavana wa kaunti ya Nairobi, Mike Sonko ameahidi kutoa mifuko isiyoathiri mazingira kwa wakazi kufanikisha shughuli ya utupaji takataka huku marufuku dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki yakiingia siku ya pili. Kwenye taarifa, Sonko alisema serikali ya kaunti ya Nairobi itaunga mkono ujenzi wa viwanda vipya na ukarabati wa vile vilivyoko kuviwezesha kutengeneza mifuko isiyoathiri mazingira. Sonko alisema hatua hiyo itatoa ajira kwa maelfu ya vijana bali na kutoa mifuko mbadala kwa wafanyibiashara na wakazi. Aliwahimiza wakazi wa kaunti ya Nairobi kulinda mazingira na kuunga mkono juhudi zake za kunadhifisha jiji la Nairobi.