Gavana Sonko atwaa kipande cha ardhi ya bustani ya city park kilichokuwa kimenyakuliwa

Gavana wa Nairobi  Mike Sonko ametwaa kipande cha ardhi ya bustani ya  City Park  ambacho kilikuwa kimenyakuliwa.  Sonko anasema kituo cha marekebisho ya tabia ambacho kimejengwa kwenye sehemu ya ardhi hiyo  kilipewa Barua ya  kugawiwa ardhi hiyo kwa njia haramu na serikali iliyotangulia. Gavana huyo aliwapa  wakurugenzi wa kituo cha  kurekebisha tabia  shilingi laki tatu na akawataka wahame eneo hilo. Hata hivyo aliwapongeza kwa kazi nzuri wanaofanya kuwarekebisha tabia watu wanaotumia mihadharati  lakini akasitika kuwa wanaendeshea shughuli zao kwenye ardhi iliyonyakuliwa.  Alisema maafisa wa kaunti waliolipatia shirika hilo lisilokuwa la serikali  Barua ya kuligawa ardhi hiyo kwa njia  isio halali wameachishwa kazi  kwa madai ya ufisadi.  Gavana huyo alisema kuwa kisima kilichokuwa kikiwahudumia wakazi wa mitaa ya  Parklands na  Westlands  na pia  shamba la ekari tano la maua la thamani ya shilingi bilioni 4.5   kwenye bustani hiyo  vimetwaliwa. Sonko alisema  pia amejitolea kulinda  ardhi ya umma  na mali na akayalaumu makundi ya wafanyabiashara wenye ushawishi mkubwa kwa  kuendeleza  unyakuzi wa ardhi.