Francis Atwoli, Ahimiza Serikali Kuingilia Kati Mara Moja Kupunguza Bei Ya Unga Wa Mahindi

Katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyikazi-COTU, Francis Atwoli, anahimiza serikali kuingilia kati mara moja kupunguza bei ya unga wa mahindi. Kwenye taarifa, Atwoli anadai kuwa madai ya wasagaji unga kwamba uzalishaji mahindi umepungua mwaka huu na kusababisha bei za unga kuongezwa ni ya kupotosha na yananuiwa kuwahadaa Wakenya kulipia zaidi chakula cha kimsingi cha ugali. Atwoli alisema uamuzi wa wasagaji mahindi hapa nchini kususia ununuzi mahindi kutoka kwa bodi ya taifa ya nafaka na mazao, wakidai kuwa mahindi hayo yameharibika ni njama dhahiri ya baadhi ya wafanyibiashara walaghai hapa nchini ya kutetea bei za juu za unga. Alisema kundi hilo la wafanyibiashara walaghai labda linataka kushinikiza uagizaji mahindi hapa nchini kutoka nje. Atwoli alihimiza serikali kuwachukulia hatua watu kama hao kwa vitendo vyao. Chama cha wasagaji nafaka kimeonya kwamba uwasilishaji haba wa mahindi unaweza kusababisha bei za unga wa mahindi kuongezwa zaidi. Kulingana na mwenyekiti wa chama hicho Nick Hutchinson, kupungua kwa uwasilishaji mahindi na uagizaji mahindi ghali kutoka nchi jirani kumesababisha kuongezeka kwa bei ya unga wa mahindi. Waziri wa kilimo Willy Bett anatarajiwa kukutana na wasagaji nafaka ili kujadili malalamishi kuhusu bei za juu za chakula hiki cha kimsingi hali ambayo imezua changamoto na kusababisha kupanda kwa gharama ya maisha.