Fracis Atwoli ataka wanasiasa kukoma kuikashifu mahakama ya juu

Katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi hapa nchini-COTU, Francis Atwoli anawataka wanasiasa wakome kuikashifu mahakama ya juu. Atwoli amesema shutma dhidi ya mahakama hiyo zinaashiria mfano mbaya wa uongozi wa nchi hii. Alisema matamshi kama hayo yanadhulumu uhuru wa idara ya mahakama. Aliongeza kwamba viongozi wanapaswa kutoa nafasi kwa idara ya mahakama kutekeleza majukumu yake bila vitisho. Akiongea katika makao makuu ya muungano wa COTU hapa Nairobi, Atwoli alivishauri vyama vya kisiasa kujianda kwa marudio ya uchaguzi wa urais mwezi novemba. Siku ya jumamosi rais Uhuru Kenyatta alikashifu vikali uamuzi wa majaji ya mahakama ya juu, hatua ambayo imezua hisia mbali mbali. Kabla ya uamuzi huo wa kihistoria siku ya ijumaa, kiongozi wa NASA, Raila Odinga pia alikuwa ameitaka mahakama ya juu kurejesha hadhi yake. Mahakama ya juu ilibatilisha matokeo ya urais na kuagiza uchaguzi mpya kuandaliwa katika muda wa siku 60.