FIDA yataka Uhuru kutimiza sheria ya jinsia ya thuluthi kwenye baraza lake la mawaziri

Shirikisho la  Wanawake Mawakili  Nchini (FIDA), limemtaka Rais  Uhuru Kenyatta kuteuwa  yamkini   wanawake saba katika kwenye baraza lake  la mawaziri  ili kutimiza sheria ya  jinsia  ya thuluthi mbili. Shirikisho hilo limesema katiba  inaeleza  kuwa  thuluthi mbili ya  viongozi  wote waliochaguliwa na kuteuliwa hawafai kuwa wa jinsia moja. Kwenye barua  ya wazi, mwenyekiti wa shirikisho  hilo  Josephine Wambua-Mong’are  alisema wako tayari kumkabidhi rais orodha ya majina  ya  wanawake wenye uwezo na waliohitimu  ambao wanaweza kuteuliwa kuwa mawaziri. Wakati huo huo, Mong’are  alisema  kujumuishwa kwa wanawake katika  uongozi kunastahili kuhusisha vyeo vyovyote vya  serikali. Alisema hatua hiyo italinda haki za wanawake na kuhakikisha wanashiriki katika utoaji maamuzi. Alitoa wito kwa Rais  Kenyatta kuyapa kipa umbele maswala  ya wanawake  na kuongeza kwamba wana matumaini rais atatii katiba anapobuni serikali mpya.  Mong’are  alisema wanasubiri kwa hamu kutangazwa kwa serikali mpya.