FBI Kujumuishwa Kwenye Uchunguzi Wa Mauaji Ya Wakili Willy Kimani Na Wenzake

Shirika la upelelezi-FBI lenye makao nchini Marekani limejumuishwa kusaidia kwenye uchunguzi wa mauaji ya wakili Willy Kimani, mteja wake na dereva wa texi mwezi uliopita. A�Mkurugenzi wa idara ya upelelezi Ndegwa Muhoro akiandamana na mkuu wa kitengo cha polisi cha Flying Squad, Munga Nyale na mkuu wa kitengo cha kukabiliana na uhalifu wa jinai walifika mahakamani jana kuwasilisha ripoti kuhusu kile asasi za usalama zinafanya kufichua mauaji hayo ya kikatili yanayohusishwa na maafisa wa polisi. Muhoro alifika mbele ya jaji Luka Kimaru na kutoa hakikisho kwamba muda wa siku 14 uliotengwa na mahakama utatoa fursa ya kufanywa uchunguzi wa kina kufichua jinsi mauaji hayo yalivyotekelezwa na utafanywa kwa njia huru huku mashahidi wakihakikishiwa ulinzi wao. Hata hivyo wakili Dkt. John Khaminiwa alishangaa ikiwa wakili huyo aliyekuwa akihudumu Nairobi aliuawa kwa sababu alifahamu mengi kuhusu huduma ya taifa ya polisi. Kampuni ya kutoa huduma za mawasiliano ya rununu ya Safaricom pia iliwasilisha mahakamani sauti za mawasiliano ya rununu na takwimu za utumaji jumbe mfupi ambazo zitachunguzwa faraghani kubainisha dakika za mwisho za waathiriwa hao watatu. Wakati huo huo afisa wa nne wa polisi anayehudumu A�katika kituo cha polisi cha Syokimau, Leonard Maina Mwangi, alifikishwa mahakamani kuhusiana na mauaji ya Kimani. Mwangi ambaye alifikishwa mbele ya hakimu Joyce Gandani ameagizwa kuzuiliwa rumande kwa siku 13 na atarejeshwa mahakamani pamoja na wanaodaiwa kuwa washirika wake watatu ambao walikuwa mahakamani hapo jana.A�A�A�A�A�A� A�