Ezekiel Mutua apongeza msako dhidi ya magari ya abiria yanayoonyesha filamu chafu

Afisa mkuu mtendaji wa Halmashauri ya kuorodhesha filamu Ezekiel Mutua amepongeza msako unaofanywa kote nchini kwenye magari ya kubeba abiria yanayoonyesha filamu chafu. Akiwahutubia wanahabari katika hoteli moja jijini Mombasa Mutua alisema msako huo unaendelea na akatoa wito kwa maafisa wa kudumisha sheria na idara ya mahakama kushirikiana na halmashauri hiyo ili kukabiliana na uovu huo.

Wakati wa msako huo uliofanywa na mratibu wa kanda wa KFCB Boniventure Kioko, maafisa wa halmashauri hiyo na polisi huko Mombasa, walinasa magari 40 ya abiria na makondakta wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani kukabiliwa na mashataka ya kuonyesha video za picha chafu. Msako huo kwenye magari ya abiria unaofanywa na halmashauri hiyo unafuatia malalamiko kutoka kwa umma ambao wameripoti visa vingi vya uonyeshaji picha chafu kwenye magari hayo ya uchukuzi wa abiria.