Emmerson Mnangagwa aapishwa leo kuwa rais wa Zimbabwe

Emmerson Mnangagwa  anatarajiwa kuapishwa leo kuwa  rais wa Zimbabwe kufwatia  hatua ya majeshi ya nchi hiyo kumwondoa mamlakani rais Robert Mugabe ambaye ametawala nchi hiyo kwa  miaka 37 na amelaumiwa kwa kutawala nchi hiyo kwa mkono mzito.Aidha inadaiwa amesambaratisha uchumi wa nchi hiyo.

Mnangagwa,ambaye alirejea nchini Zimbabwe siku ya jumatano kutoka uhamishoni baada ya kufutwa kazi na rais Mugabe, na kushangiliwa kwa vifijo na nderemo, ataapishwa kwenye uwanja mmoja wa michezo mjini Harare.Kutimuliwa kwake uongozini ni mongoni mwa sababu zilizosababisha majeshi ya nchi hiyo kumwondoa uongozini.Mugabe ,mwenye umri wa miaka 93 alikuwa amekataa kujiuzulu ,lakini baada ya shinikizo kutoka kwa raia na majeshi ,alikubali kung’atuka   mamlakani.Upinzani unamtaka Mnangagwa ambaye ni kigogo wa vita vya ukombozi wa Zimbabwe kuwa msitari wa mbele kuupiga vita ufisadi ambao umekithiri nchini humo na kuchukua hatua za kukwamua uchumi wa taifa hilo,ambalo kwa wakati mmoja lilikuwa linajitosheleza kwa chakula.