Emmerson Mnangagwa achukua rasmi uongozi wa Zimbabwe

Emmerson Mnangagwa ndiye rais mpya wa Zimbabwe baada ya kuapishwa kuhudumu mahala pa rais Robert Mugabe aliyeondolewa mamlakani. Mnangagwa ameapishwa mchana wa leo na jaji mkuu wa nchi hiyo, Luke Malaba katika hafla iliyohudhuriwa na maelfu ya raia wa Zimbabwe mjini Harare. Umati mkubwa ulikusanyika katika uwanja wa michezo wa kitaifa katika mji mkuu wa Zimbabwe wa Harare, kushuhudia kuapishwa kwa Emmerson Mnangagwa kuwa rais wa nchi hiyo. Viongozi mbali mbali kutoka barani walihudhuria hafla hiyo.