Eddy Gicheru Oketch akubali ushindi wa Ayako

Mgombea uchaguzi wa chama cha Federal Party of Kenya, Eddy Gicheru Oketch, amekiri kushindwa kwenye uchaguzi mdogo wa useneta wa Migori uliokamilika hivi punde. Oketch aliibuka wa pili kwa kura 60,555 nyuma ya Ochillo Ayacko wa chama cha ODM ambaye alishinda uchaguzi huo kwa kura 85,234. Oketch aliwashukuru wafuasi wake ambao walisimama pamoja naye.

Hata hivyo, alilalamikia kuvamiwa vituo vya kupigia kura na viongozi wa chama cha ODM wasio wa kaunti ya Migori. Oketch alisema haya baada ya matokeo kutangazwa na afisa wa usimamizi wa uchaguzi huko Migori Ruth Kulundu katika chuo cha waalimu cha Migori. Kwenye hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi, Ayacko aliwashukuru wakazi wa Migori kwa kuwa na imani naye na kumchagua kwa wingi wa kura. Ayacko aliapa kuwaunganisha wakazi wa Migori na kuwahudumia kwa usawa licha ya miegemeo yao ya kisiasa. Uchaguzi mdogo huo hata hivyo ulikumbwa na kujitokeza idadi ndogo ya wapiga kura. Asilimia 28.02 ya wapiga kura 388,333 waliosajiliwa huko Migori walijitokeza kushiriki kwenye uchaguzi huo. Kiti hicho kilibakia wazi kufuatia kifo cha seneta Ben Oluoch mwezi Juni mwaka huu.