Maafisa wa afya katika hali ya tahadhari kufuatia kuzuka kwa Ebola Congo

Maafisa wa afya nchini wako katika hali ya tahadhari kufuatia kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola katika jamhuri ya kidemokrasia yaA�A�Congo ambao kufikia sasa umesababisha vifo vya watu watatu. Wizara ya afya imesema kuwa imefungua tena vituo vya uchunguzi kwenye viingilio vya humu nchini katika juhudi za kuzuia virusi vya ugonjwa huo kuingizwa humu nchini. Hata hivyo imesema kuwa hakuna sababu yoyote ya kuhofu. Ugonjwa huo umezuka katika jamhuri hiyo ambapo tayari watu watatu wamefariki na wengine sita kulazwa hospitalini. Ingawa serikali inasisitiza kwamba ugonjwa huo umezuka kwenye eneo moja la mbali kwenye jamhuri hiyo na hatua kabambe zimechukulia, wizara ya afya imesema kuwa imechukua hatua sawa na zile ilizochukua mwaka 2014 wakati ugnjwa huo ulipozuka katika eneo la Afrika magharibi ili kuhakikisha hakuna hatari ya virusi hivyo kuingizwa humu nchini. Kadhalika wizara hiyo imepeleka maafusa wa kushughulikia dharura ili kuimarisha uchunguzi na kuwafuatilia wasafiri walio na viwango vya juu vya joto na wale ambao husafiri mara kwa mara kutoka au kupitia jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na pia kuwachunguza wasafiri kutoka au wanaopitia kwenye jamhuri hiyo katika vituo vyote vya kuingia humu nchini. Kadhalika vyumba maalum vimetengwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta ili kuwatenga watu wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo. Vile vile huduma za ugunduzi wa magonjwa katika taasisi ya KEMRI, na vituo vya kuwatenga na kuwahudumia wagonjwa kwenye hospitali ya kitaifa ya Kenyatta na vituo vingine vya afya nchini vimewekwa katika hali ya tahadhari ili kuimarisha uwezo wa kugundua na kuchukua hatua kuhusiana na visa vyovyote vinavyoshukiwa kuwa vya maambukizi ya ugonjwa huo humu nchini.