EACC Yapata Ushahidi Zaidi Unaohusisha Gavana Kidero Na Ufisadi

Uchunguzi uliofanywa na tume ya maadili na vita dhidi ya ufisadi unafichua kwamba huenda gavana wa Nairobi, Evans Kidero, alishawishi idara ya mahakama kwenye rufaa iliyopinga uchaguzi wake. Hati ya kiapo iliyotayarishwa na tume ya kupambana na ufisadi inadokeza kwamba, Kidero alipokea zaidi ya shilingi milioni 317 zikiwa akiba za pesa taslimu katika mojawapo ya akaunti zake kati ya mwezi Januari mwaka wa 2011 na mwezi Disemba mwaka wa 2015. Rufani hiyo inasema akaunti hiyo pia inaonyesha kiasi cha shilingi milioni 200 ambazo ni sawa na zaidi ya dolla milioni 2 ambazo ziliwekwa katika akaunti thabiti. Tume ya kupambana na ufisadi kwenye utathmini wake ilisema Kidero angeliweza kulipa kwa urahisi shilingi milioni 200 ambacho ni kiasi sawa na kile kinasemekana kilitumiwa kuwashawishi majaji kwenye kesi ya rufani ili kumpendelea. Tume ya vita dhidi ya ufisadi pia imegundua akaunti nyingine zinazohusishwa na gavana Kidero ambazo imeanza kuzichunguza. Tume ya EACC inakiri kwamba Kidero huenda alihusika kwenye ufisadi na uhalifu wa kiuchumi kwani taarifa za benki zinaonyesha kiasi kikubwa cha fedha kikiwekwa akiba kati akaunti mara kwa mara hali ambayo ni sawa na ulanguzi wa pesa.