Duale apongeza Wabunge waliohudumu baada ya uhuru

Wabunge waliohudumu punde baada ya nchi hii kunyakua uhuru wake wamepongezwa kwa uadilifu wao licha ya kwamba hawakuwa na vifaa na manufaa kama yale yaliyoko kwa sasa. Kiongozi wa walio wengi Aden Duale alisema wabunge hao hawakufurahia manufaa kama vile hazina ya ustawi wa maeneo bunge na mikopo ya ununuzi magari na nyumba lakini walifaulu katika utekelezaji majukumu yao ya utathmini utenda kazi wa serikali, utungaji sheria na uwakilishi maslahi ya Wakenya. Duale alikuwa akichangia hoja ya kuwaidhinisha makamishna walioteuliwa kuhudumu katika tume ya kuwaajiri wafanyikazi wa bunge. Miongoni mwa wabunge walioteuliwa kuwa makamishna wa tume hiyo ni Naomi Shaban wa Taita Taveta, Aden Keynan wa Eldas ,Ben Momanyi wa Borabu na Aisha Jumwa wa Malindi. Wengine ni maseneta Beth Mugo ambaye ni seneta maalum, Aaron Cheruiyot wa Kericho na George Khaniri wa Vihiga. Kadhalika kiongozi wa wengi aliwakumbusha makamishna hao wapya kuhakikisha kwamba bunge haliajiri wafanyikazi wasio na uadilifu akiongeza kusema kwamba ipo haja ya kufanya utathmini wa wafanyikazi wa bunge. Kiongozi wa walio wachache John Mbadi na mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi walisema tume ya kuwaajiri wafanyikazi wa bunge ina wajibu mkubwa wa A�kuwawezesha wabunge na wafanyikazi wa bunge kutekeleza majukumu yao.