Donald Trump ashutumu rais wa Syria

Rais wa Marekani Donald Trump, ameshutumu rais wa Syria Bashar al-Assad kwa kupita mipaka baada ya kuwashambulia raia kwa gesi ya sumu. Trump alisema shambulizi hilo limebadili msimamo wake kuhusiana na serikali hiyo lakini hakubainisha hatua atakazochukua. Alisema shambulizi hilo lililosababisha vifo vya watu 70 wengi wao wakiwa watoto linahitaji kuchukuliwa hatua, matamshi ambayo yanaambatana na yale ya aliyekuwa rais Barack Obama aliyetishia kuishambulia Syria kupitia angani ikiwa itatekeleza shambulizi kama hilo. Matamshi hayo yamejiri siku chache baada ya Marekani kusema haina nia ya kumlazimisha Assad kuondoka mamlakani. Hata hivyo huenda yakaibua upya mzozo kati ya Marekani na Urusi ambazo zilikuwa zimeanza kuonesha dalili za kusitisha uhasama.