Donald Trump asema Umoja wa Mataifa haujaafikia uwezo wake kikamilifu

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Umoja wa Mataifa haujaafikia uwezo wake kikamilifu kutokana na urasimu na usimamizi duni. Katika hotuba yake ya kwanza katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, alitoa wito wa kulenga zaidi raia kuliko urasimu. Akishtumu kile alichokielezea kuwa mzigo mkubwa wa kifedha ambao umetwikwa Marekani, Trump alisema Umoja wa mataifa ungekuwa imara zaidi iwapo wanachama wangelishirikiana ipasavyo. Marekani huigharimia aslimia 22 ya jumla ya bajeti ya Umoja wa mataifa na aslimia 28 ya gharama za ulindaji wa amani duniani. Kiongozi huyo wa Marekani anatarajiwa leo kutoa hotuba ndefu kwa mara ya kwanza kwenye kikao cha baraza kuu la Umoja huo. Anatarajiwa kutoa mwito wa kuchukuliwa msimamo mkali dhidi ya mataifa ya Korea kaskazini na Iran. Kwenye kikao maalum kuhusu marekebisho kwenye umoja huo, Trump alizitaka nchi wanachama kuchukua mzimamo usio wa kawaida zinapoyashughulikia maswala ya umoja huo.