Dkt. Amoth aagiza madereva wote wa Malori kutoka Tanzania kupimwa Corona

Madereva wote wa malori kutoka Tanzania watakuwa wakipimwa upya humu nchini kuhakikisha kwamba hawana virusi vya Corona.

Kaimu Mkurugenzi wa Afya katika Wizara ya Afya Dkt. Patrick Amoth, aliagiza hayo huku akipuuzilia mbali madai ya Tanzania kwamba matokeo ya vipimo hivyo nchini siyo sahihi.

Akiwahutubia wanahabari huko Namanga,kaunti ya Kajiado, Dkt. Amoth alisema mahabara ya nyanjani iliyoko kwenye mpaka kati ya nchi hizo inaweza kupima takriban sampuli 600 kila siku.

Alisema wakazi wote katika eneo hilo la mpakani watapimwa kubaini iwapo wana virusi vya Corona.

Wakati huo huo,wakazi wa Namanga wamehimiza serikali kufunga mpaka kati ya Kenya na Tanzania ili kuzuia kuenea kwa virusi vya Corona.

Wito huo unajiri kufuatia kuongezeka kwa visa vya maradhi ya COVID-19 nchini Tanzania.