Diane Shima Rwigara mpinzani mkuu wa serikali nchini Rwanda atiwa nguvuni

Polisi nchini Rwanda wamemtia nguvuni Diane Shima Rwigara mwanaharakati  na mpinzani mkuu wa serikali  kwa tuhuma za kughushi stakabadhi na kukwepa kulipa ushuru. Aidha mama yake na dada yake walitiwa  mbaroni siku ya Jumatatu kwa tuhuma za kukwepa kulipa ushuru. Awali  mwaka huu, maafisa wa uchaguzi  walimzuia Rwigara  kuwania  wadhifa wa urais, ambao rais Paul Kagame alishinda kwa kura nyingi, kwa misingi kwamba hakuwasilisha idadi ya kutisha ya saini  kutoka kwa wafwasi wake. Aidha tume hiyo ilisema kuwa baadhi ya saini alizowasilisha ni za majina ya watu waliofariki. Hata hivyo Rwigara alikanusha madai hayo. Rwigara, mwenye umri wa miaka 35, ambaye ni mhasibu kwa taaluma alimlaumu rais Kagame kwa kuwazima wapinzani wake na kushutumu  chama cha Rwanda Patriotic Front  kwa kuhodhi mamlaka. Alidai kuwa amekuwa kwenye kizuizi cha nyumbani kabla ya kutiwa nguvuni   na polisi jana.