Dereva Aliyesababisha Ajali Kisii Akamatwa

nyamagwa

Dereva wa basi la shule lililokumbwa na ajali na kusababisha vifo vya wanafunzi wanne wa shule ya upili ya wasichana ya St Marya��s Nyamagwa katika kaunti ya Kisii yuko korokoroni akisubiri kukamilishwa kwa uchunguzi kuhusu ajali hiyo.

Mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya kitaifa ya uchukuzi na usalama barabarani, Francis Meja amesema dereva huyo, Erick Gituma Muthenya ambaye ni mfanyikazi wa kampuni ya Associated Motors anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Ogembo huku maafisa wa polisi wakiendelea na uchunguzi.

Kamanda wa polisi kaunti ya Kisii, Agnes Mudambah alisema dereva huyo huenda akakabiliwa na mashtaka kadhaa yakiwemo kusababisha vifo kupitia uendeshaji gari kiholela. Naye naibu mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya NTSA, Benjamin Kibogong amesema Muthenya alikuwa akiendesha gari hilo kwa kasi likiwa na abiria kupita kiasi alipopoteza mwelekeo.

Katibu katika wizara ya elimu, Belio Kipsang alisema kwenye taarifa kuwa wanafunzi-20 wangali katika hospitali ya Kisii Level 6. Kwa niaba ya wizara ya elimu, Dr Kipsang alituma rambi rambi kwa jamaa na marafiki wa wasichana wanne waliopoteza maisha kweenye ajali hiyo.