Dereva afariki katika ajali ya barabara nchini Ufaransa

Dereva wa gari moja alifariki mapema leo baada ya gari hilo kugonga malori yaliyokuwa yamesimama kwenye barabara moja karibu na bandari ya Calais kaskazini mwa ufaransa ambako wahamiaji walikuwa wamefunga barabara kwa magogo ya miti. Gari hilo lililokuwa na nambari za usajili za Poland lilishika moto lilipogonga malori hayo. Uraia wa dereva huyo haukubainika mara moja. Afisa mmoja wa serikali katika eneo hilo alisema kuwa wahamiaji tisa kutoka Eritrea waliopatikana kwenye mojawapo wa malori hayo ya kubebea mizigo yaliyokwama kwenye kizuizi hicho cha barabarani walikamatwa na kuzuiliwa. Kwa miaka kadhaa eneo la Calais limekuwa mapito ya wahamiaji kutoka mashariki ya kati na bara Afrika wanaojaribu kuelekea nchini uingereza kinyume cha sheria.